Ken Walibora: Mtoto Wa Mama


Siku moja nitawadia- na nitarudi kuko huko moyo wangu uliko, na labda maisha tena nitayatamani… na hiyo itakuwa siku njema kwangu. 

Profesa Ken Walibora
Ken Walibora. Kituoni NTV.

Japo kaenda kule kuliko hatima ya maisha, Ken Waliaula Walibora atasalia nyoyoni mwetu kama mwanalugha na gwiji ambaye kalamu yake daima itatiririka kwa wino wa tumaini. Nisemavyo sibuni namna alivyosimulia yeye mwenyewe katika hadithi ya Maskini Babu Yangu. Ken si jina la vitabuni tu wala sauti redioni- wapo kina Sylvester Jack Oyoo na Hassan Ali, wote watangazaji- bali ni fingo la uandishi katika lugha yenye uhondo si haba.

Shaaban bin Robert katutia imani kuwa titi la mama li tamu jingine haliishi hamu, Alamin Mohamed Mazrui katushawishi kuwa haki ina kilio, Euphrase Kezilahabi katukumbusha kuwa lugha haina budi kusomeka na kutumika, Wallah bin Wallah katupa ngeli ila nala ya uandishi katupa Ken Waliaula Walibora, mtoto wa mama!

Vitabuni na nakalani nilimsikia tangia mwaka wa 2005 alipotajwa mara kwa mara na amu yangu. Kumsoma mwenyewe nilianza mnamo mwaka wa 2010; Siku Njema ikiwa riwaya funguzi ikifuatiwa na hadithi fupi ya Tuzo katika mkusanyiko wa Mayai Waziri wa Maradhi na Hadithi Nyingine, Ndoto ya Almasi, Kufa Kuzikana, Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine na maandishi mengine anuwai.

Katika Siku Njema, Kongowea Mswahili anaufungua mdahalo wa swala la mwanaharamu pamoja na maana ya jina ‘baba’; hakuna aliye mwanaharamu ingawa baba huenda ni neno lililojipata kamusini kama dosari. Babake, Juma Mukosi, mwenyewe alikuwa msomi wa kupigiwa mfano. Hata hivyo, ulimwengu ulimkimbia; ama tuseme, aliukimbia ulimwengu. Kwa kawaida binadamu huvurugika wakati mmoja au zaidi na huenda akajipata kusiko na jua wala mwanga. Basi Juma Mukosi kabadili jinale likawa Amuj Isokum. Amuj si jina la msimbo namna tunavyojibandikia majina.

Upevu wa Kidagaa Kimemwozea u wazi. Kitambo hakijapita tangu gatuzi la jiji la Nairobi likabidhiwe usukani wake Mkurugenzi Mkuu. Basi aliyekuwa katibu alisinzia kisha kaupa mji mgongo. Upo wakati karani katika hazina ya wafanyakazi alisafiri kwa ndege kila siku licha ya mshahara punje alioupokea. Kweli hana anachotamani! Maabadi yamepagawa kwa makuhani wasiompa Mola kicho. Kabla ya uhasama wa kisiasa, rais alimteua bingwa fulani aliyeyapa masomo mgongo katika darasa la saba kuwa Waziri wa Michezo.

Ama kweli, vipofu ndio rubani! 

Kufa Kuzikana
Kufa Kuzikana (Life Buddies). Riwaya yake

Tufe tufaane hata urafiki wetu uwe wa Kufa Kuzikana. Vita vya kikabila vilichipuka nchini Kenya na Rwanda katika mwongo wa 90. Zilikuwa ni enzi zilizojawa na mchafuko na uhasama usio kipimo. Watu walipigana, jamii zilitengana nazo habari zilipeperushwa. Akida Sululu anapoteza ufadhili wa kujiunga na shule ya upili pamoja na kupotea kwa diwani yake babake. Hata hivyo, njia yafunguka hatimaye kwake kuelekea Kanada. 

Ndoto Ya Almasi

Ufukara huumbua na kufedhehesha. Japo binadamu akakosa imani ya kuishi, umaskini katu haukubaliki. Almasi kasingiziwa kwa kosa asilolifahamu kamwe nayo ndoto yake ya kuwa msomi ikazimwa ghafla. Hata hivyo, Ndoto ya Almasi yatushawishi kutathmini namna tunavyowashughulikia viongozi wa kesho hasa kwa kuwaandalia leo iliyo kamili.

Walibora ameviandika vitabu vingi nami nimezidiwa na ukwasi wa maneno kuvielezea. Hata hivyo, mshumaa ushawaka nasi hatuna budi ila kuuangazia na kutembea palipo nuru.

Ajabu hino ajabu, ya nyangumi kufa maji!~ Ken Walibora

 

Na Kefa Simiyu

Alhamisi, Aprili 16, 2020

 

 

Published by econscholaruon

Not only is the concept of 'free' a 'lie' but a morass; a price of zero signifies a return to the barter system which we left behind when we did away with the Stone Age. We cause change that transforms.

One thought on “Ken Walibora: Mtoto Wa Mama

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Design a site like this with WordPress.com
Get started