Siku Njema na Ken Walibora: Darubini La Uchumi


Binadamu daima katelekezwa na minyororo ya kujikimu, nao mtaji ndio leseni yake. Tangia utotoni hadi ukomavu, kazi, japo iwe ya sulubu ama yenye kumdhalilisha, ni bidii ya mja. Wapo wale huchumia juani wakikusudia kulia kivulini. Baadhi ya insi ya vinyemelea huku wengine siku zao zote watundika nambari nne miguuni; swala la kazi kwao ni ndoto tupu namna ilivyo kwenye filamu ya Disney World.

Kizazi kimoja huekeza kwa manufaa ya vizazi vya halafu. Ufukara na hali ya nikiulizwa siungami hurithiwa katika familia zisizoekeza. Ili kufukiza baridi ya umaskini, familia hohehahe huukumbatia uroda. Hivyo basi, ni nadra kushuhudia uchache wa wana kokote kuliko na lindi la mtambo.

Babuye Kongowea Mswahili alikuwa na vikembe tisini licha ya mti wa utajiri kumparama. Kutokana na hali ngumu kiuchimi, wengi wao hawakufanikiwa kushiriki skuli. Basi kisomo walichokipokea kilitokana na ukarimu wa shule ya maisha. Wangozi husema kuwa asiyefunzwa na mama hufunzwa na ulimwengu. Ama tuseme kusoma kwa namna hii hakupendezi au tajriba ya maisha huja na mchakato wa maovu si haba.

Hadi kufa kwake, mamake Kongowea, Zainabu, alikuwa mwimbaji mashuhuri katika bendi mojs ya taarabu. Hata hivyo, sifa pasi na pesa hazisaidi. Zainabu alijing’atua bendini huku azima yake ikiwa kuistawisha hatima ya mwanawe. Juma Mukosi alivutia na unyoofu wa sauti, umilisi wa lugha tamu na sura yake Zainabu. Basi akamchumbia na mwishowe wakaushtaki ukapera. Zainabu vilevile alivutiwa na kisomo chake Juma Mukosi ambacho bila shaka kilikuwa kikombozi. Isitoshe, aliamini kuwa mzawa wao sharti awe na akili zisizofika shule. Vigoli na wanawake kwa jumla huvutiwa na wavulana ama wanaume werevu na wenye maarifa.

Kitabu kilimtambua Msanifu Kombo nayo masomo yakamkubali. Darasani hakuwahi kosa miongoni mwa wanafunzi bora. Wapo watu waliouhusisha umahiri huu na ushirikina. Suleimani Mapunda, kwa mfano, alilaani kuwa Msanifu kampokonya bahati masomoni. Ama ikubalike kuwa imani yake ilimjuvya kuwa hang’amui lolote shuleni maadamu yupo gwiji au iwe kuwa Suleimani Mapunda kazaliwa bongo lala. Bibiye mjombake aliamini vivyo hivyo kuwa watoto wake si wasomi maadamu binamu kaiiba bahati yao kielimu. Jambo hili liliukuza uhasama kati yake Msanifu Kombo na Suleimani Mapunda na mkewe mjomba.

Bi Rahma alikabidhiwa siri ya aliko babake Msanifu naye Zainabu. Bi Rahma naye kasuhubiana na mkewe mjomba baada ya kifo chake Zainabu. Hatimaye, kamtobolea siri na mipango kabambe kuanzishwa ili Enoch, jamaa wake, aende kuupokea urithi wa bandia. Kufunga safari kwake Enoch kulifahamishwa na imani ya kufua dafu. Kando na hayo, kuwepo kwake mrithi halali hakukumshurutisha akatize safari yake. Kwa bahati mbaya ama njema, Enoch kafa katika ajali barabarani.

Kwingineko, mkewe mjomba anakusudia kumsumu Msanifu maanake kuwepo kwake kulikuwa mzigo katika kiambo hicho. Hata hivyo, Vumilia binti Abdala anamfichulia siri hiyo na kumwongoa Kongowea. Ingawa yaweza tajwa kuwa Vumilia alimwokoa Kongowea kutokana na utu wake au upendo aliomwelekelezea- hata shuleni daima alimtetea Kongowea kila mara alipochokozwa kwa kuitwa kikochozi- Vumilia alim’enzi kama mume kufuu yake katika siku za halafu. Ama kweli, aliiokoa ndoa na nyumba yake. Ndiposa wasomi wengi wa riwaya ya Siku Njema hawashtuki katu Kongowea anapomwoa Vumilia.

Siku moja Bi Rahma kavamia na fahali alipokuwa akitoka marikiti. Kongowea ndiye kamwauni kwa kumfukuza yule fahali. Bi Rahma anafunguka roho na kumsimulia usuli wake. Hafanyi hivyo kama jambo lisiloepukika! Kwake Rahma, uhai ulizidi usuhuba wake na mkewe mjomba. Alipoyapima maswala hayo mawili, aliupata uhai ukawa na uzani usiomithilika. Zaidi ya hayo, alimsaidia Kongowea katika shughuli za maandalizi hayo kisiri. Ningependa kuandika na kueleza mengi ila nina hofu nisije nikajitungia riwaya.

 

 

Na Kefa Simiyu

Jumatatu, Aprili 20, 2020

Published by econscholaruon

Not only is the concept of 'free' a 'lie' but a morass; a price of zero signifies a return to the barter system which we left behind when we did away with the Stone Age. We cause change that transforms.

One thought on “Siku Njema na Ken Walibora: Darubini La Uchumi

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

Design a site like this with WordPress.com
Get started